1 Usihangaike kwa sababu ya waovu;usiwaonee wivu watendao mabaya.
2 Maana hao watatoweka mara kama nyasi;watanyauka kama mimea mibichi.
3 Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kutenda mema,upate kuishi katika nchi na kuwa salama.
4 Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu,naye atakujalia unayotamani moyoni.
5 Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako;mtumainie yeye naye atafanya kitu.
6 Ataufanya wema wako ungae kama mwanga,na uadilifu wako kama jua la adhuhuri.
7 Tulia mbele ya Mwenyezi-Mungu, mngojee kwa saburi;usihangaike juu ya wale wanaofanikiwa,watu wanaofaulu katika mipango yao mibaya.
8 Epuka hasira wala usiwe na ghadhabu;usihangaike maana hiyo huzidisha ubaya.
9 Watu watendao mabaya wataangamizwa,bali wanaomtumaini Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi.
10 Bado kitambo kidogo, naye mwovu atatoweka;utamtafuta pale alipokuwa, wala hutamwona.
11 Lakini wapole wataimiliki nchi,hao watafurahia wingi wa fanaka.
12 Mwovu hula njama dhidi ya mwadilifu,na kumsagia meno kwa chuki.
13 Lakini Mwenyezi-Mungu humcheka mwovu,kwani ajua mwisho wake u karibu.
14 Waovu huchomoa panga na kuvuta pinde zao,wapate kuwaua maskini na fukara;wawachinje watu waishio kwa unyofu.
15 Lakini panga zao zitawapenya wao wenyewe,na pinde zao zitavunjwavunjwa.
16 Afadhali mali kidogo ya mtu mwadilifukuliko utajiri wa watu waovu wengi.
17 Maana nguvu za waovu zitavunjwa,lakini Mwenyezi-Mungu huwategemeza waadilifu.
18 Mwenyezi-Mungu hutunza maisha ya watu waaminifu,na urithi wao utadumu milele.
19 Hawataaibika zikifika nyakati mbaya;siku za njaa watakuwa na chakula tele.
20 Lakini waovu wataangamia,maadui za Mwenyezi-Mungu watanyauka kama maua nyikani;naam, watatoweka kama moshi.
21 Mtu mwovu hukopa bila kurudisha;lakini mwadilifu hutoa kwa ukarimu.
22 Waliobarikiwa na Mwenyezi-Mungu wataimiliki nchi,lakini waliolaaniwa naye watafutiliwa mbali.
23 Mwenyezi-Mungu huziongoza nyayo za mtu,humlinda yule ampendezaye.
24 Ajapoanguka, haanguki akabaki chini,kwa sababu Mwenyezi-Mungu humtegemeza.
25 Nilikuwa kijana na sasa ni mzee;kamwe sijaona mwadilifu ameachwa na Mungu,au watoto wake wakiombaomba chakula.
26 Daima huwapa wengine kwa furaha na kukopesha,na watoto wake ni baraka.
27 Achana na uovu, utende mema,nawe utaishi nchini daima;
28 maana Mwenyezi-Mungu hupenda uadilifu,wala hawaachi waaminifu wake.Huwalinda hao milele;lakini wazawa wa waovu wataangamizwa.
29 Waadilifu wataimiliki nchi,na wataishi humo milele.
30 Mtu mwadilifu husema maneno ya hekima,kwa ulimi wake hunena yaliyo ya haki.
31 Huizingatia moyoni mwake sheria ya Mungu wake;naye hatetereki katika mwenendo wake.
32 Mtu mwovu humvizia mtu mwema na kujaribu kumuua;
33 lakini Mwenyezi-Mungu hatamtia mtu mwema makuchani mwake,wala kumwacha apatilizwe akishtakiwa.
34 Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kushika njia yake,naye atakukuza uimiliki nchi,na kuwaona waovu wakiangamizwa.
35 Nilimwona mwovu mdhalimu sana,alijiweka juu ya wote kama mierezi ya Lebanoni!
36 Baadaye nikapita hapo, naye hakuwapo tena;nikamtafuta, lakini hakuonekana tena.
37 Mwangalie mtu mwema, mtu mwadilifu;mtu anayependa amani hujaliwa wazawa.
38 Lakini wakosefu wote wataangamizwa;na wazawa wao watafutiliwa mbali.
39 Mwenyezi-Mungu huwaokoa waadilifu,na kuwalinda wakati wa taabu.
40 Mwenyezi-Mungu huwasaidia na kuwaokoa;huwatoa makuchani mwa waovu na kuwaokoa,maana wanakimbilia usalama kwake.