1 Mbingu zatangaza utukufu wa Mungu;anga ladhihirisha kazi ya mikono yake.
2 Mchana waupasha habari mchana ufuatao,usiku waufahamisha usiku ufuatao.
3 Hamna msemo au maneno yanayotumika;wala hakuna sauti inayosikika;
4 hata hivyo, sauti yao yaenea duniani kote,na maneno yao yafika kingo za ulimwengu.Mungu ameliwekea jua makao yake angani;
5 nalo hutoka kama bwana arusi chumbani mwake,lafurahi kama shujaa aliye tayari kushindana.
6 Lachomoza toka upande mmoja,na kuzunguka hadi upande mwingine;hakuna kiwezacho kuliepa joto lake.
7 Sheria ya Mwenyezi-Mungu ni kamilifu,humpa mtu uhai mpya;masharti ya Mwenyezi-Mungu ni thabiti,huwapa hekima wasio na makuu.
8 Kanuni za Mwenyezi-Mungu ni sawa,huufurahisha moyo;amri ya Mwenyezi-Mungu ni safi,humwelimisha mtu.
9 Kumcha Mwenyezi-Mungu ni jambo jema,na la kudumu milele;maagizo ya Mwenyezi-Mungu ni sawa,yote ni ya haki kabisa.
10 Yatamanika kuliko dhahabu;kuliko dhahabu safi kabisa.Ni matamu kuliko asali;kuliko asali safi kabisa.
11 Yanifunza mimi mtumishi wako;kuyafuata kwaniletea tuzo kubwa.
12 Lakini nani aonaye makosa yake mwenyewe?Ee Mungu, niepushe na makosa nisiyoyajua.
13 Unikinge mimi mtumishi wako na makosa ya makusudi,usikubali hayo yanitawale.Hapo nitakuwa mkamilifu,wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa.
14 Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu,yakubalike mbele yako, ee Mwenyezi-Mungu,mwamba wangu na mkombozi wangu!