Zaburi 35 BHN

Kuomba msaada

(Zaburi ya Daudi)

1 Ee Mwenyezi-Mungu, uwapinge hao wanaonipinga;uwashambulie hao wanaonishambulia.

2 Utwae ngao yako na kingio lako,uinuke uje ukanisaidie!

3 Chukua mkuki na sime yako dhidi ya wanaonifuatia.Niambie mimi kwamba utaniokoa.

4 Waone haya na kuaibika,hao wanaoyanyemelea maisha yangu!Warudishwe nyuma kwa aibu,hao wanaozua mabaya dhidi yangu.

5 Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo,wakikimbizwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu!

6 Njia yao iwe ya giza na utelezi,wakifukuzwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu!

7 Maana walinitegea mitego bila sababu;walinichimbia shimo bila kisa chochote.

8 Maangamizi yawapate wao kwa ghafla,wanaswe katika mtego wao wenyewe,watumbukie humo na kuangamia!

9 Hapo mimi nitafurahi kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu;nitashangilia kwa kuwa yeye ameniokoa.

10 Nitamwambia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote:“Wewe ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliye kama wewe!Wewe wawaokoa wanyonge makuchani mwa wenye nguvu,maskini na fukara mikononi mwa wanyanganyi.”

11 Mashahidi wakorofi wanajitokeza;wananiuliza mambo nisiyoyajua.

12 Wananilipa mema yangu kwa mabaya;nami binafsi nimebaki katika ukiwa.

13 Lakini wao walipokuwa wagonjwa,mimi nilivaa magunia kuonesha huzuni;nilijitesa kwa kujinyima chakula.Nilisali nikiwa nimeinamisha kichwa,

14 kana kwamba namlilia rafiki au ndugu yangu.Nilikwenda huko na huko kwa huzuni,kama mtu anayeomboleza kifo cha mama yake.

15 Lakini mimi nilipoanguka walikusanyika kunisimanga.Walikusanyika pamoja dhidi yangu.Watu nisiowajua walinirarua bila kukoma,wala hakuna aliyewazuia.

16 Watu ambao huwadhihaki vilema,walinisagia meno yao kwa chuki.

17 Ee Mwenyezi-Mungu, utatazama tu mpaka lini?Uniokoe kutoka kwenye mashambulio yao;uyaokoe maisha yangu na simba hao.

18 Hapo nitakushukuru kati ya kusanyiko kubwa la watu;nitakutukuza kati ya jumuiya kubwa ya watu.

19 Usiwaache maadui hao wabaya wanisimange,hao wanichukiao bure wafurahie mateso yangu.

20 Maneno wasemayo si ya amani,wanazua maneno ya hila dhidi ya wananchi watulivu.

21 Wananishtaki kwa sauti:“Haya! Haya! Tumeona wenyewe uliyotenda!”

22 Lakini wewe Mwenyezi-Mungu waona jambo hilo,usinyamaze, ee Mwenyezi-Mungu,usikae mbali nami.

23 Uinuke, ee Mwenyezi-Mungu, ukanitetee;uje, ee Mungu wangu, uangalie kisa changu.

24 Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, unitetee,ufanye kulingana na uadilifu wako;usiwaache maadui zangu wanisimange.

25 Usiwaache wajisemee: “Tumefanikiwa tulivyotaka!”Au waseme: “Tumemmaliza huyu!”

26 Waache hao wanaofurahia maafa yangu,washindwe wote na kufedheheka.Hao wote wanaojiona wema kuliko mimi,waone haya na kuaibika.

27 Lakini wanaotaka kuona kuwa sina hatia,wapaaze sauti kwa furaha waseme daima:“Mwenyezi-Mungu ni mkuu mno!Hupendezwa na fanaka ya mtumishi wake.”

28 Hapo nami nitatangaza uadilifu wako;nitasema sifa zako mchana kutwa.