1 Nakupenda, ee Mwenyezi-Mungu, nguvu yangu!
2 Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu,ngome yangu na mkombozi wangu;Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia usalama;ngao yangu, nguvu za wokovu wangu na ngome yangu.
3 Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie,nami naokolewa kutoka kwa maadui zangu.
4 Kamba za kifo zilinizingira,mawimbi ya maangamizi yalinivamia;
5 kamba za kuzimu zilinizinga,mitego ya kifo ilinikabili.
6 Katika taabu yangu nilimwita Mwenyezi-Mungu,nilimlilia Mungu wangu anisaidie.Aliisikia sauti yangu hekaluni mwake;kilio changu kilimfikia masikioni mwake.
7 Hapo dunia ikatetemeka na kutikisika;misingi ya milima ikayumbayumba,kwani Mungu alikuwa amekasirika.
8 Moshi ulifuka kutoka puani mwake,moto uunguzao ukatoka kinywani mwake;makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake.
9 Aliinamisha anga, akashuka chini;na wingu jeusi chini ya miguu yake.
10 Alipanda kiumbe chenye mabawa akaruka;akapaa kasi juu ya mabawa ya upepo.
11 Alijifunika giza pande zote,mawingu mazito yaliyojaa maji yalimzunguka.
12 Umeme ulimulika mbele yake;kukatokea mawinguni mvua ya mawe na makaa ya moto.
13 Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni;Mungu Mkuu akatoa sauti yake,kukatokea mvua ya mawe na makaa ya moto.
14 Aliwapiga maadui mishale yake, akawatawanya,alirusha umeme, akawatimua.
15 Ulipowakemea maadui zako ee Mwenyezi-Mungu,ulipowatisha kwa ghadhabu yako,vilindi vya bahari vilifunuliwa,misingi ya dunia ikaonekana.
16 Mungu alinyosha mkono kutoka juu akanichukua,kutoka katika maji mengi alininyanyua.
17 Aliniokoa kutoka kwa maadui zangu wenye nguvu nyingi,aliniokoa kutoka kwa hao walionichukia,maana walikuwa na nguvu kunishinda.
18 Walinivamia nilipokuwa taabuni,lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa kinga yangu.
19 Alinileta, akaniweka mahali pa usalama;alinisalimisha, kwani alipendezwa nami.
20 Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu;alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia.
21 Maana nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu,wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu.
22 Nimeshika maagizo yake yote,sikuacha kufuata masharti yake.
23 Mbele yake sikuwa na hatia;nimejikinga nisiwe na hatia.
24 Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu;yeye ajua kwamba mikono yangu haina hatia.
25 Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu;mwema kwa wale walio wema.
26 Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu;lakini mkatili kwa watu walio waovu.
27 Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu,lakini wenye majivuno huwaporomosha.
28 Wewe ee Mwenyezi-Mungu, waniangazia;walifukuza giza langu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.
29 Kwa msaada wako nakishambulia kikosi;wewe wanipa nguvu ya kuruka ukuta.
30 Huyu Mungu matendo yake hayana dosari!Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika;yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia usalama.
31 Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu?Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu?
32 Mungu ndiye anijaliaye nguvu kila upande;ndiye anayeifanya salama njia yangu.
33 Ameiimarisha miguu yangu kama ya paa,na kuniweka salama juu ya vilele.
34 Hunifunza kupigana vita,mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba.
35 Umenipa ngao yako ya kuniokoa;mkono wako wa kulia umenitegemeza;wema wako umenifanikisha.
36 Umenirahisishia njia yangu;wala miguu yangu haikuteleza.
37 Niliwafuatia adui zangu na kuwakamata;sikurudi nyuma mpaka nimewaangamiza.
38 Niliwaangusha chini wasiweze kuinuka tena;walianguka chini ya miguu yangu.
39 Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita;uliwaporomosha maadui chini yangu.
40 Uliwafanya maadui zangu wakimbie,na wale walionichukia niliwaangamiza.
41 Walipiga yowe lakini hapakuwa na wa kuwaokoa;walimlilia Mwenyezi-Mungu lakini hakuwajibu.
42 Niliwatwanga wakawa kama vumbi inayopeperushwa na upepo;niliwakanyaga kama tope la njiani.
43 Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu,ukanifanya mtawala wa mataifa.Watu nisiowajua walinitumikia.
44 Mara waliposikia habari zangu walinitii.Wageni walinijia wakinyenyekea.
45 Wageni walikufa moyo;wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka.
46 Mwenyezi-Mungu yu hai!Asifiwe mwamba wa usalama wangu;atukuzwe Mungu wa wokovu wangu.
47 Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi;na kuyashinda mataifa chini yangu.
48 Ameniokoa kutoka kwa maadui zangu,akanikuza juu ya wapinzani wangu,na kunisalimisha mbali na watu wakatili.
49 Kwa hiyo nitakutukuza kati ya mataifa,ee Mwenyezi-Mungu nitaliimbia sifa jina lako.
50 Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa;humwonesha fadhili zake huyo mteule wake,naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.