1 Ee Mwenyezi-Mungu, kwako naielekeza nafsi yangu!
2 Nakutumainia wewe, ee Mungu wangu,usiniache niaibike;adui zangu wasifurahie kushindwa kwangu.
3 Usimwache anayekutumainia apate aibu;lakini waaibike wote wanaokuasi kwa makusudi.
4 Unijulishe njia zako, ee Mwenyezi-Mungu;unifundishe nifuate unayotaka.
5 Uniongoze katika ukweli wako na kunifundisha,kwani wewe ni Mungu, mwokozi wangu;ninakutegemea wewe kila siku.
6 Uikumbuke huruma yako ee Mwenyezi-Mungu;uzikumbuke na fadhili zako kuu,ambazo zimekuwako tangu kale.
7 Usikumbuke dhambi na makosa ya ujana wangu;unikumbuke kadiri ya fadhili zako,kwa ajili ya wema wako, ee Mwenyezi-Mungu.
8 Mwenyezi-Mungu ni mwema na mnyofu,kwa hiyo huwafundisha wenye dhambi njia.
9 Huwaongoza wanyenyekevu katika uadilifu;naam, huwafundisha hao njia yake.
10 Mwenyezi-Mungu hutenda kwa fadhili na uaminifu,kwa wale wanaoshika agano lake na maamuzi yake.
11 Kwa ajili ya jina lako, ee Mwenyezi-Mungu,unisamehe kosa langu kwani ni kubwa.
12 Kila mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu,Mwenyezi-Mungu atamfunza njia ya kufuata.
13 Mtu wa namna hiyo atafanikiwa daima,na wazawa wake watamiliki nchi.
14 Mwenyezi-Mungu ni rafiki ya wale wamchao;yeye huwajulisha hao agano lake.
15 Namwangalia Mwenyezi-Mungu daima;yeye atainasua miguu yangu mtegoni.
16 Unielekee, ee Mungu, unionee huruma,maana mimi ni mpweke na mnyonge.
17 Uniondolee mahangaiko ya moyoni mwangu;unitoe katika mashaka yangu.
18 Uangalie mateso yangu na dhiki yangu;unisamehe dhambi zangu zote.
19 Angalia jinsi walivyo wengi maadui zangu;ona jinsi wanavyonichukia kwa ukatili.
20 Uyalinde maisha yangu, uniokoe;nakimbilia usalama kwako,usikubali niaibike.
21 Wema na uadilifu vinihifadhi,maana ninakutumainia wewe.
22 Ee Mungu, uwaokoe watu wako, Israeli;uwaokoe katika taabu zao zote.