1 Ee Mwenyezi-Mungu, usinikemee kwa hasira yako;usiniadhibu kwa ghadhabu yako.
2 Unihurumie, ee Mwenyezi-Mungu, nimeishiwa nguvu;uniponye, ee Mwenyezi-Mungu, nataabika mpaka mifupani.
3 Ninahangaika sana rohoni mwangu.Ee Mwenyezi-Mungu, utakawia mpaka lini?
4 Unigeukie, ee Mwenyezi-Mungu, uniokoe;unisalimishe kwa sababu ya fadhili zako.
5 Huko kwa wafu hakuna anayekukumbuka;huko kuzimu ni nani awezaye kukusifu?
6 Niko hoi kwa kilio cha uchungu;kila usiku nalowesha kitanda changu kwa machozi;kwa kulia kwangu naulowesha mto wangu.
7 Macho yangu yamechoka kwa huzuni;yamefifia kwa kutaabishwa na adui.
8 Ondokeni kwangu enyi nyote watenda maovu!Maana Mwenyezi-Mungu amesikia kilio changu.
9 Mwenyezi-Mungu amesikia ombi langu;Mwenyezi-Mungu amekubali sala yangu.
10 Maadui zangu wote wataaibika na kufadhaika;watarudi nyuma na kuaibishwa ghafla.