1 Ee Mwenyezi-Mungu, unitetee,maana nimeishi bila hatia,nimekutumainia wewe bila kusita.
2 Unijaribu, ee Mwenyezi-Mungu, na kunipima;uchunguze moyo wangu na akili zangu.
3 Fadhili zako ziko mbele ya macho yangu,ninaishi kutokana na uaminifu wako.
4 Sijumuiki na watu wapotovu;sishirikiani na watu wanafiki.
5 Nachukia mikutano ya wabaya;wala sitajumuika na waovu.
6 Nanawa mikono yangu kuonesha sina hatia,na kuizunguka madhabahu yako, ee Mwenyezi-Mungu,
7 nikiimba wimbo wa shukrani,na kusimulia matendo yako yote ya ajabu.
8 Ee Mwenyezi-Mungu, napenda makao yako,mahali unapokaa utukufu wako.
9 Usiniangamize pamoja na wenye dhambi,wala usinitupe pamoja na wauaji,
10 watu ambao matendo yao ni maovu daima,watu ambao wamejaa rushwa.
11 Lakini mimi ninaishi kwa unyofu;unihurumie na kunikomboa.
12 Mimi nimesimama mahali palipo imara;nitamsifu Mwenyezi-Mungu katika kusanyiko kubwa.