1 Nitakushukuru Mungu kwa moyo wangu wote;nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.
2 Nitafurahi na kushangilia kwa sababu yako;nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mkuu.
3 Wakati ulipotokea, maadui zangu walirudi nyuma,walijikwaa na kuangamia.
4 Umenitetea kuhusu kisa changu cha haki;umeketi katika kiti chako cha enzi,ukatoa hukumu iliyo sawa.
5 Umeyakemea mataifa,umewaangamiza waovu;majina yao umeyafutilia mbali milele.
6 Maadui wameangamia milele;umeingolea mbali miji yao,kumbukumbu lao limetoweka.
7 Lakini Mwenyezi-Mungu anatawala milele;ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.
8 Anauhukumu ulimwengu kwa haki;anayaamua mataifa kwa unyofu.
9 Mwenyezi-Mungu ni ngome ya watu wanaoonewa;yeye ni ngome nyakati za taabu.
10 Wanaokujua wewe, ee Mungu hukutegemea,wewe Mwenyezi-Mungu huwatupi wakutafutao.
11 Mwimbieni sifa Mwenyezi-Mungu akaaye Siyoni.Yatangazieni mataifa mambo aliyotenda!
12 Mungu hulipiza kisasi kwa umwagaji damu;kamwe hasahau kilio cha wanaoonewa.
13 Unirehemu, ee Mwenyezi-Mungu!Ona mateso ninayoteswa na wanaonichukia;wewe waninyakua kutoka nguvu za kifo,
14 nisimulie sifa zako mbele ya watu wa Siyoni,nipate kushangilia kwa sababu umeniokoa.
15 Watu wa mataifa wametumbukia katika shimo walilochimba,wamenaswa miguu katika wavu waliouficha.
16 Mwenyezi-Mungu amejionesha alivyo;ametekeleza hukumu.Watu waovu wamenaswa kwa matendo yao wenyewe.
17 Waovu wataishia kuzimu;naam, mataifa yote yanayomsahau Mungu.
18 Lakini fukara hawatasahauliwa daima;tumaini la maskini halitapotea milele.
19 Inuka, ee Mwenyezi-Mungu!Usimwache binadamu ashinde.Uyakusanye mataifa mbele yako, uyahukumu.
20 Uyatie hofu, ee Mwenyezi-Mungu,watu wa mataifa watambue kuwa wao ni watu tu!