5 Mnaangua mayai ya joka lenye sumu,mnafuma utando wa buibui.Anayekula mayai yenu hufa,na yakipasuliwa nyoka hutokea.
6 Utando wenu haufai kwa mavazi,watu hawawezi kujifunikia mnachofuma.Kazi zenu ni kazi za uovu,matendo yenu yote ni ukatili mtupu.
7 Mko mbioni kutenda maovu,mnaharakisha kumwaga damu isiyo na hatia.Mawazo yenu ni mawazo ya uovu,popote mwendapo mnaacha ukiwa na uharibifu.
8 Njia ya amani hamwijui kamwe;njia zenu zote ni za dhuluma.Mmejifanyia njia potovu,yeyote anayepitia humo hapati amani.
9 Ndio maana haki iko mbali nasi,maongozi ya uadilifu hayapo kwetu.Tunatazamia kupata mwanga kumbe ni giza tupu,twatazamia mwangaza, lakini twatembea gizani.
10 Kama vipofu twapapasapapasa ukuta;tunasitasita kama watu wasio na macho.Tunajikwaa mchana kana kwamba ni usiku,miongoni mwa wenye nguvu sisi ni kama wafu.
11 Twanguruma kama dubu,twaomboleza tena na tena kama hua.Twatazamia hukumu ya haki, lakini haipo,twatazamia wokovu, lakini uko mbali nasi.