Zab. 107 SUV

KITABU CHA TANO

Shukrani kwa Kukombolewa katika Dhiki

1 Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema,Kwa maana fadhili zake ni za milele.

2 Na waseme hivi waliokombolewa na BWANA,Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi.

3 Akawakusanya kutoka nchi zote,Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini.

4 Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika;Hawakuona mji wa kukaa.

5 Waliona njaa, waliona na kiu,Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao.

6 Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,Akawaponya na shida zao.

7 Akawaongoza kwa njia ya kunyoka,Wapate kwenda mpaka mji wa kukaa.

8 Na wamshukuru BWANA, kwa fadhili zake,Na maajabu yake kwa wanadamu.

9 Maana hushibisha nafsi yenye shauku,Na nafsi yenye njaa huijaza mema.

10 Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti,Wamefungwa katika taabu na chuma,

11 Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu,Wakalidharau shauri lake Aliye juu.

12 Hata akawadhili moyo kwa taabu,Wakajikwaa wala hakuna msaidizi.

13 Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,Akawaponya na shida zao.

14 Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti,Akayavunja mafungo yao.

15 Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake,Na maajabu yake kwa wanadamu.

16 Maana ameivunja milango ya shaba,Ameyakata mapingo ya chuma.

17 Wapumbavu, kwa sababu ya ukosaji wao,Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa.

18 Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula,Wameyakaribia malango ya mauti.

19 Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,Akawaponya na shida zao.

20 Hulituma neno lake, huwaponya,Huwatoa katika maangamizo yao.

21 Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake,Na maajabu yake kwa wanadamu.

22 Na wamtolee dhabihu za kushukuru,Na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba.

23 Washukao baharini katika merikebu,Wafanyao kazi yao katika maji mengi,

24 Hao huziona kazi za BWANA,Na maajabu yake vilindini.

25 Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba,Ukayainua juu mawimbi yake.

26 Wapanda mbinguni, watelemka vilindini,Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya.

27 Wayumba-yumba, wapepesuka kama mlevi,Akili zao zote zawapotea.

28 Wakamlilia BWANA katika dhiki zao,Akawaponya na shida zao.

29 Huituliza dhoruba, ikawa shwari,Mawimbi yake yakanyamaza.

30 Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametuliaNaye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani.

31 Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake,Na maajabu yake kwa wanadamu.

32 Na wamtukuze katika kusanyiko la watu,Na wamhimidi katika baraza ya wazee.

33 Amegeuza mito ikawa jangwa,Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu.

34 Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi,Kwa sababu ya ubaya wao walioikaa.

35 Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji,Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji.

36 Maana amewakalisha huko wenye njaa,Nao wametengeneza mji wa kukaa.

37 Wakapanda mbegu katika mashamba,Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake.

38 Naye huwabariki wakaongezeka sana,Wala hayapunguzi makundi yao.

39 Kisha wakapungua na kudhilika,Kwa kuonewa na mabaya na huzuni.

40 Akawamwagia wakuu dharau,Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia.

41 Akamweka mhitaji juu mbali na mateso,Akamfanyia jamaa kama kundi la kondoo.

42 Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi,Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa.