1 Njoni, tumwimbie BWANA,Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
2 Tuje mbele zake kwa shukrani,Tumfanyie shangwe kwa zaburi.
3 Kwa kuwa BWANA ni Mungu mkuu,Na Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
4 Mkononi mwake zimo bonde za dunia,Hata vilele vya milima ni vyake.
5 Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya,Na mikono yake iliumba nchi kavu.
6 Njoni, tuabudu, tusujudu,Tupige magoti mbele za BWANA aliyetuumba.
7 Kwa maana ndiye Mungu wetu,Na sisi tu watu wa malisho yake,Na kondoo za mkono wake.Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
8 Msifanye migumu mioyo yenu;Kama vile huko MeribaKama siku ya Masa jangwani.
9 Hapo waliponijaribu baba zenu,Wakanipima, wakayaona matendo yangu.
10 Miaka arobaini nalihuzunika na kizazi kile,Nikasema, Hao ni watu waliopotoka mioyo,Hawakuzijua njia zangu.